
Katika ujumbe wake, Hizbullah imesisitiza dhamira ya kuishi kwa amani na kuunga mkono jeshi na taifa la Lebanon katika kukabiliana na uvamizi. Harakati hiyo imesema vitendo vya Israel ni uvamizi usiokubalika.
“Tunategemea msimamo wa utakatifu wako katika kukataa dhulma na uvamizi unaofanywa dhidi ya taifa letu la Lebanon na wavamizi wa Kizayuni,” taarifa iliongeza.
Taarifa hiyo imetolewa wakati wa ziara ya Papa Leo XIV nchini Lebanon ambayo inaanza Jumapili ya leo huku ikitarajiwa kujumuisha mikutano na viongozi wa kiraia na kidini, ziara ya misikiti na makanisa ya kale, sala katika bandari ya Beirut kwa kumbukumbu ya waathirika wa mlipuko wa 2020, na mkutano binafsi na Rais Joseph Aoun.
Papa pia atapanda mti wa mwerezi katika ikulu ya rais na kusali katika kaburi la Mtakatifu Charbel na mbele ya sanamu ya Mama Yetu wa Lebanon.
Katibu Mkuu wa Hzibullah Sheikh Naim Qassem amekaribisha ziara hiyo, akisisitiza kuwa kundi lake limezingatia makubaliano ya kusitisha vita ya Novemba 2024, na kutaka mashambulizi ya Israel yakome.
Makubaliano hayo yalihitaji Israel kujiondoa kikamilifu katika ardhi ya Lebanon, lakini bado imeweka vikosi katika maeneo matano, kinyume na Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 1701.
Tangu utekelezaji wa makubaliano hayo, Israel imekiuka mara kadhaa kwa mashambulizi ya mara kwa mara. Viongozi wa Lebanon wameonya kuwa ukiukaji huo unatishia uthabiti wa taifa.
3495566